MUMMY'S MAN
Alichosema mama kwa Kijana wake wa kiume siku moja kabla ya kufunga ndoa.
Mummy’s man!
Wewe sasa ni mwanaume. Kuanzia kesho utakuwa na mwanamke mwigine wa maisha yako. Mpishi mwingine na mtu mwingine wa kushare nae siri zako, sitakuwa mimi tena.
Mpende mwanamke wako pengine kuliko hata mimi. Kabla hujaenda jumla kuanza maisha mengine mwanangu acha nikupe maneno machache yatakayokuongoza;
Kuna siku nilikuwa sina maelewano mazuri na baba yako. Nilikuwa nikipiga kelele na kufoka hasira zilikuwa juu, nae hasira zake zilikua juu vilevile. Nikamtusi kwa kumwambia yeye ni "mpumbavu".
Alinishangaa!! Akaniuliza nathubutuje kumuita yeye mpumbavu? Hapo hapo nikamuongezea matusi mengine nikimuita mjinga, na hana busara, nilimuita majina yote mabaya.
Angalia unajua ni nini alifanya? Hakunyanyua mkono wake kunipiga. Aliondoka kimya kimya. Akabamiza mlango na kutokomea.
Mwanangu, kama baba yako angenipiga labda na kuniumiza, kunivunja either mkono au mguu, ungekaa na mimi hapa? Ungemuheshimu kama baba yako? Je ungekuwa unajivunia kuwa na baba kama yeye? Au ungenilaumu mimi kwa kumuita yale majina ya kuudhi.
Kamwe usimpige mkeo! Haijalishi amekuudhi kwa kiasi gani. Wewe kaa kimya na ondoka na mambo yatasonga. Kila atakapojaribu kuleta maudhi kumbuka haya niliyokueleza.
Kabla sijasahau, Baada ya baba yako kuondoka, nilijisikia vibaya mno. Alirudi akiwa bado na hasira. Na asubuhi siku iliyofuata nilifanya kila naloweza kumuomba msamaha.
Alinisamehe kwa moyo mweupe na siku hiyo nilimpikia chakula kizuri akipendacho, Yes najua unafahamu kuwa baba yako anapenda sana mboga za maboga zilizochanganywa na viazi mbatata.
Baada ya siku hiyo sikumuita tena majina ya kuudhi wala kumkasirisha. Heshima yangu kwake ilizidi maradufu.
Kuna kitu kikubwa cha muhimu ambacho unahitajika kukifanya kila siku, mwanangu nisikilize, mtetee mke wako.
Pale atakapokuwa under pressure simama nae kidete. Kama marafiki zako watamchukia ni jukumu lako kumfanya ajione kama ni malkia wa nguvu.
Baba zako wakubwa na wadogo hawakuwahi kunipenda, lakini baba yako siku zote alisimama upande wangu mpaka pale walipokuja kubadilika na kuniomba msamaha.
Kuna siku baba yako alikuwa mwenyeji wa mmiliki wa kampuni pamoja na wafanyakazi wenzake wawili alikokua akifanyia kazi, wote waliomba kujihifadhi hapa nyumbani kwetu.
Siku hiyo nilikuwa jikoni nikiwapikia chakula na baba yako alienda kununua vinywaji kwa ajili ya wageni. Baada ya kumaliza na kuandaa chakula mezani, kila mmoja alianza kula.
Ndipo nikakumbuka kuwa nilisahau kuweka chumvi katika chakula. Niliaibika mno mbele ya wageni. Baba yako baada ya kula tu kijiko cha kwanza alinitizama. Halafu hapohapo akawatazama wageni.
Akawaambia wageni kwamba alinipa maelekezo mwezi uliopita kwamba nisiwe naweka chumvi katika chakula kwa vile ana matatizo ya kiafya. Alizungumza hayo kwa utani mwingi na bashasha kuizima ile aibu.
Wageni walielewa na akaniomba niende nikachukue chumvi kila mmoja ajiwekee kivyake. Yeye alikula vilevile bila chumvi mpaka akamaliza. Baada ya wageni kuondoka alinihimiza tu kwa upole kuwa makini siku nyingine.
Mke wako ni kama mtoto, muda mwingine anaweza akashindwa cha kuongea au cha kufanya. Simama na ongea kwa ajili yake!
Tengeneza mazoea ya kwenda maeneo mbalimbali na mkeo, hiyo inampa ujasiri na kujiamini. Mbali na kazini, tembelea maeneo mengine na yeye.
Kama kuna mtu atakualika nyumbani kwake, au katika event yoyote ile na akakwambia usiende na mkeo kuwa makini na utumie busara.
Najua unanipenda mimi mama yako, najua huwa unanieleza matatizo na changamoto zako. Lakini kwa sasa mambo ni tofauti.
Mkeo awe wa kwanza kujua hayo kabla hujanieleza mimi. Mwache yeye aone kabla yangu.
Kama unamatatizo nae usikimbilie kwangu. Acha siku ipite na uongee nae mwenyewe, na uombe Mungu kwa ajili ya hilo jambo.
Usishirikishe marafiki zako matatizo ya mkeo, kwao itakuwa burudani na watakucheka kinafiki kwa kushindwa kusimamia ustawi wa ndoa yako.
La mwisho, usisahau kuja kunitembelea wewe na mkeo kila mwezi. Najua utakuwa na nyumba yenye furaha, ila siku zote wewe bado ni mummy's Man.
Mungu atabariki nyumba yako na uzao wako. Usisahau kumuomba yeye na kutafuta msaada kwake.
Nimekulea katika maadili mema, Nimekusomesha, una elimu kubwa, basi ukawe mfano bora kwa kila kijana ulimwenguni, ukawatie moyo na kuwapa matumaini juu ya Ndoa.
Msingi wa taifa lolote lenye maadili huanzia katika ngazi ya familia. Hii ambayo wewe unaenda kuijenga.
Nitakupenda siku zote mwanangu, nenda na ninakutakia kila la kheri mwenyezi Mungu akubariki wewe, mkeo mtarajiwa na uzao wako.
Nakupenda mwanangu, sehemu ya nyama zangu. Enenda kwa amani.